Ijumaa, 11 Septemba 2015

SOMO LA ASUBUHI LEO

MATENDO MEMA HUONGEZEKA KWA KUYAFANYIA MAZOEZI 


Katika mambo yote ukijionyesha wewe mwenyewe kuwa kielelezo cha matendo mema, na katika mafundisho yako ukionyesha usahihi na ustahivu, na maneno yenye uzima yasiyoweza kuhukumiwa makosa, ili yule mwenye kupinga atahayarike, kwa kuwa hana neno baya la kunena juu yetu. Tito 2:7, 8.

Mkristo mwenye afya, anayeendelea kukua hatakuwa mpokeaji anayekaa tu bila kutenda lo lote akiwa miongoni mwa wenzake. Yampasa kutoa na vile vile kupokea. Matendo yetu mema huongezeka kwa kuyafanyia mazoezi. Jamii ya Kikristo itatupatia hewa safi ya kuvuta, na katika kuivuta kwetu hatuna budi kuwa na juhudi. Kazi ya Kikristo ifanyike, huruma zetu, kuwatia moyo wengine, na mafundisho vitolewe nasi kwa wale wanaohitaji, kujizuia, upendo, uvumilivu, na ustahimilivu ambavyo huhitajika, vikitumika katika kazi hii ya Kikristo, vitajenga ndani yetu wenyewe imani, utii, tumaini, na upendo kwa Mungu wetu.... Ni jambo la maana ili kuwa na musuli wa kiroho na nguvu kwamba roho iwe na mazoezi. Kazi inapaswa kufanywa kwa utendaji wa kiroho tukizitumia vizuri nafasi za kufanya mema.... Kadiri mtu anavyozidi kuwa mwaminifu katika kufanya kazi zake za Kikristo, ndivyo atakavyozidi kuwa mkamilifu....

Udhaifu na kutokuwa na msimamo wo wote havitatupatia kamwe heshima yo yote katika imani yetu ya Kikristo. Haiwezekani kuwafikia watu kule waliko na kuwainua juu isipokuwa kama tumaini fulani limeamshwa ndani yao kwa njia ya uaminifu na utauwa wako. Huwezi kamwe kuwafikia kwa kushuka chini ya jukwaa hilo la kweli na matengenezo, isipokuwa kwa kuwaleta wengine juu ya jukwaa hilo ambalo Neno la Mungu limekuandalia wewe. Iwapo watu wale wanaoipinga imani yetu wanaona kwamba ninyi mnaoikiri hamna utani, yaani, mko imara, wala hamna tabia mbaya kwa nyakati zote na chini ya hali zote, na ya kwamba mnakaa ndani ya Kristo, Mzabibu hai, na ya kwamba ninyi ni wafuasi wa ile kweli na wafanya matengenezo msioyumba, hapo ndipo mtakapoakisi roho na tabia ile ya Kristo. Katika biashara zenu, katika ushirikiano wenu na waumini pamoja na wale wasio waumini, katika patakatifu [kanisani], nyumbani mwenu, na kila mahali, hapo ndipo mtakapoonyesha mvuto wa upendo wake Mwokozi, ambao utawatawala waumini.

Kipaji, talanta, na fedha sio vya muhimu ili kuweza kuwa na mvuto huo; lakini jambo la maana ni kwamba wewe ukae ndani yake Kristo, maana kwa njia hiyo matunda yako yatakuwa ya haki. ----- Letter 1, 1882.

Alhamisi, 10 Septemba 2015

SOMO LA ASUBUHI LEO

RAFIKI KWA WALE WASIOKUWA NA RAFIKI 


Marhamu na manukato huufurahisha moyo; Kadhalika utamu wa rafiki ya mtu utokao katika kusudi la moyo wake. Mithali 27:9.

Ingetupasa sisi kuwa na upendo wa Kristo moyoni mwetu kwa kiwango kile ambacho kuwapenda wengine kutakuwa kwa haki na unyofu. Mapenzi yetu yangekuwa na upeo mpana, wala yasingewekwa tu kwa wachache wanaojipendekeza kwetu kwa kutuambia siri zao muhimu. Mwelekeo wa urafiki kama huo ni kutufanya tuwasahau wale walio na hitaji kubwa la kupendwa kuliko wale ambao mawazo yetu yanaelekea kwao.

Jumatano, 9 Septemba 2015

SOMO LA ASUBUHI LEO

YAKUPASA KUCHAGUA KUNDI LAKO


Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema Bwana, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha. 2 Wakorintho 6:17.

Mkristo wa kweli hatachagua kundi la wale ambao hawajaongoka. Iwapo Kristo ameumbika ndani, tumaini la utukufu, hatuwezi kufurahia hali ya hewa yenye malaria ya kiroho ambayo inazizunguka roho za wale wanaoipinga dini....

Jumanne, 8 Septemba 2015

SOMO LA ASUBUHI LEO

CHUNGA MAPENZI YAKO.


Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza? 2 Wakorintho 6:14.

Ningependa kukuonya* ujilinde kuhusu ni wapi unayaweka mapenzi yako.... Kumbuka kwamba maisha yako ni mali yake Yesu, na ya kwamba haikupasi kuishi kwa ajili ya nafsi yako tu. Haikupasi kuingia katika uhusiano wa ndoa na mtu asiyekuwa muumini, maana kwa kufanya hivyo, unafanya kinyume kabisa na kile alichoagiza Yesu. Waepuke wale wasioyaheshimu mambo ya dini. Mwepuke yule apendaye kukaa kivivu; mwepuke yule anayeyadhihaki mambo matakatifu. Epuka kushirikiana na yule anayetumia lugha chafu, au mwenye mazoea ya kutumia hata gilasi moja tu ya kileo kikali. Usisikilize posa ya mtu ambaye hautambui wajibu wake kwa Mungu.

Jumatatu, 7 Septemba 2015

SOMO LA ASUBUHI LEO

UWE NA UWEZO WA KUCHAGUA! 


Wala msishirikiane na matendo yasioyozaa ya giza, bali myakemee. Waefeso 5:11.
Mkristo anapaswa kujitenga mbali na kundi la wale ambao ni kama mtego kwa roho yake. Unapokutana na wale usioweza kuwainua katika hali ile ya hewa iliyo safi na takatifu kwa sababu mwelekeo wao wa kimaadili umepotoka, itakupasa kuwaepuka usishirikiane nao. Watu wa tabaka hiyo kwa kawaida wana utashi wenye nguvu na tabia inayovutia, na yule adui wa Mungu anapowashughulikia, wanakuwa mawakala wake wanaofanikiwa sana katika kuziongoza roho za watu mbali na njia ile ya haki na kwenda katika njia zile za udanganyifu na za hatari. Hali ya hewa ya kimaadili inayowazunguka watu hao imetiwa waa la dhambi, nayo inaleta kwa wengine shinikizo la mvuto unaonajisi. ----- YI, Sept. 29, 1892.

Jumapili, 6 Septemba 2015

SOMO LA ASUBUHI LEO

HEWA SAFI YA MAADILI 


Ili upate kwenda katika njia ya watu wema, Na kuyashika mapito ya wenye haki. (Mithali 2:20).

Ili kuwa na mwili wenye afya, ni lazima damu izungukayo katika mishipa iwe safi; ili ipate kuwa safi ni lazima ipate hewa safi na chakula safi. Matumizi ya chakula kisichofaa na uvutaji wa hewa chafu huleta ugonjwa ambao hujitokeza katika hali mbalimbali.

Jumamosi, 5 Septemba 2015

SOMO LA ASUBUHI LEO

HARUFU NZURI KATIKA KAZI YETU YA MAISHA


Na mavazi, ya nini kuyasumbukia? Fikirini maua ya mashamba, jinsi yameavyo; hayafanyi kazi, wala hayasokoti, nami nawaambia, ya kwamba hata Sulemani katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo la hayo. Mathayo 6:28,29.

Msanii wetu Mkuu anayageuza mawazo yetu kuelekea kwenye maua ya mashamba yasiyokuwa na roho, akituonyesha rangi zake nzuri na aina mbalimbali za rangi ambazo ua moja linaweza kuwa nazo. Kwa njia hiyo, Mungu ametufunulia ustadi na utunzaji wake. Hivyo ndivyo ambavyo angelionyesha pendo lake alilo nalo kwa kila mwanadamu. ----- 5BC 1086.

Ijumaa, 4 Septemba 2015

SOMO LA ASUBUHI LEO

MABWAWA MAKUBWA YA MUNGU 


Kabla haijazaliwa milima, wala hujaiumba dunia, Na tangu milele hata milele ndiwe Mungu. (Zaburi 90:2).

Baba yetu wa Mbinguni ametupatia ishara nyingi zinazoonyesha ukuu wake na utukufu wake. Jambo hilo ni hivyo hasa kwa kiwango cha kustaajabisha katika sehemu hizi za milima....* Mandhari mbalimbali katika milima hii mirefu sana na miinuko yake yenye miamba, makorongo ya milima hii yenye kina kirefu pamoja na vijito vyake vya maji vinavyokwenda kasi na kupiga kelele toka juu ya milima hii, ... maji yake yakipasuka yanapogonga miamba, na kutawanyika katika rasharasha kama mtandio, huifanya mandhari hiyo kuwa nzuri kupita kiasi na yenye utukufu ajabu....

Alhamisi, 3 Septemba 2015

SOMO LA ASUBUHI LEO Alhamisi, Septemba 3, 2015

SHULE YA AKILI NA MAADILI 


Nao wauimba wimbo wa Musa, mtumwa wa Mungu, na wimbo wa Mwana-Kondoo, wakisema, Ni makuu, na ya ajabu, matendo yako, Ee Bwana Mungu Mwenyezi; Ni za haki, na za kweli, njia zako, Ee Mfalme wa mataifa. (Ufunuo 15:3.)

Mwasisi Mkuu ameumba na kuzitengeneza mandhari mbalimbali katika maumbile [ulimwengu huu] ili zipate kuwa na maana kubwa katika tabia ya mwanadamu kiakili na kimaadili. Hizo zinatakiwa ziwe shule ya Mungu ya kuikuza akili na maadili. Hapo ndipo akili inaweza kuwa na nyanja pana sana ya utafiti katika maonyesho hayo ya matendo makuu ya Mungu wa milele. Miamba ni miongoni mwa vitu vya thamani ulimwenguni, ikiwa na hazina za hekima na maarifa. Katika miamba na milima hiyo umeandikwa ukweli kwamba hakika Mungu aliwaangamiza kwa Gharika wale waovu juu ya uso wa nchi hii. ----- MS 73, 1886.

Jumatano, 2 Septemba 2015

SOMO LA ASUBUHI LEO Jumatano, Septemba 1, 2015

VIUMBE VYA ASILI HUMTANGAZA MUNGU 


Nimezikumbuka siku za kale, Nimeyatafakari matendo yako yote, Naziwaza kazi za mikono yako. Nakunyoshea mikono yangu; Nafsi yangu inakuonea kiu kama nchi kame. (Zaburi 143:5,6.)

Tumeiangalia milima mirefu sana yenye matuta ya mkingamo katika uzuri wake mkuu, pamoja na buruji zake za miamba zinazofanana na nyumba kubwa za zamani zenye boma [ngome]. Milima hiyo hututangazia sisi ghadhabu ya Mungu iangamizayo ili apate kuithibitisha sheria yake iliyovunjwa; kwa maana [milima hiyo] iliinuliwa juu kwa tetemeko lililoitikisa sana nchi wakati ule wa Gharika. Ni kama mawimbi yenye nguvu nyingi sana yaliyosimama wakati yaliposikia sauti ya Mungu ----- mawimbi yaliyogandishwa, yaliyozuiwa katika kiburi chake kikubwa sana na kuwa mawimbi makubwa. Milima hiyo mirefu sana ni yake Mungu; anakaa juu ya ngome za miamba yake iliyo imara. Utajiri unaotokana na migodi yake ni wake pia, na hivyo ndivyo vilivyo mali yake vilindi vile virefu vya nchi.