Jumatano, 21 Oktoba 2015

SOMO LA ASUBUHI LEO

JE, NINAMWAKILISHA BWANA WANGU IPASAVYO?


Ninyi ni mashahidi wangu, asema BWANA, na mtumishi niliyemchagua.( Isaya 43:10).

Iwapo waumini wanafanya urafiki na wale wasioamini kwa kusudi la kuwaleta kwa Kristo, basi, watakuwa mashahidi wake Kristo, na baada ya kutekeleza utume wao huo, watajitenga ili kuvuta hewa safi na takatifu. Wataweza kumkaribia Mungu, na kupeleka dua zao juu kwa Kristo kwa niaba ya rafiki zao na wale wanaoshirikiana nao, wakijua kwamba anaweza kuwaokoa kabisa wale wote wamjiao Mungu kwa yeye.

Unapokuwa katika jamii ya wasioamini, kumbuka daima kwamba kwa tabia yako wewe u mwakilishi wake Yesu Kristo, usiruhusu maneno ya kipuuzi, na yale yasiyo na maana, yaani, maongezi ya kipuuzi, kutoka kinywani mwako. Zingatia thamani ya roho ya mtu, nawe kumbuka kwamba ni haki yako na wajibu wako kwa kila njia inayowezekana kuwa mtenda kazi pamoja na Mungu. Usijishushe hadhi yako ili upate kuwa sawa na wale wasioamini, na kucheka na kusema maneno yasiyo na maana kama wao wanavyofanya. Kwa kufanya hivyo... unajiweka katika hali moja na mwenye dhambi yule. Mwenendo kama huo utakufanya uwe kikwazo katika njia ya wenye dhambi....