Jumatano, 11 Novemba 2015

SOMO LA ASUBUHI LEO

CHUNGU CHA MAJARIBU MAKALI YATAKAYOLETA TAABU


Ole! maana siku ile ni kuu, hata hapana inayofanana nayo, maana ni wakati wa taabu yake Yakobo; lakini ataokolewa nayo. Yeremia 30:7.

Njia inayoleta uhuru kutoka dhambini ni ile ya kuisulubisha nafsi, na kupambana na nguvu zile za giza. Na asiwepo mtu ye yote wa kukatishwa tamaa kwa sababu ya maonjo makali watakayokutana nayo katika kipindi kile cha wakati wa taabu ya Yakobo ambacho kiko mbele yao. Wanapaswa kufanya kazi kwa bidii, kwa wasiwasi, si kwa ajili ya wakati ule, bali kwa leo hii. Tunachotaka ni kupata maarifa ya ile kweli kama ilivyo katika Kristo hivi sasa, na kuwa na uzoefu sasa kila mmoja wa kwake [wa maisha yale ya ushindi dhidi ya kila dhambi]. Katika saa hizi za thamani za kufungia mlango wa rehema, tunapaswa kuwa na uzoefu huo wenye kina na ulio hai. Kwa njia hiyo, tutajenga tabia zile zitakazotuhakikishia kuokolewa kwetu katika wakati ule wa taabu.

Wakati wa taabu ni chungu cha majaribu makali ambacho kitazidhihirisha [ndani ya watu wake] tabia zile zinazofanana na ile ya Kristo. Kimekusudiwa kuwaongoza watu wa Mungu wafikie mahali pa kumkataa Shetani na majaribu yake. Pambano lile la mwisho litamfunua kwao Shetani kwa tabia yake halisi, yaani, ile ya mtawala katili anayetumia mabavu, nalo litawafanyia mambo yale ambayo hakuna kitu kingine cho chote ambacho kingeweza kuyafanya, yaani, kumng'oa kabisa [Shetani] kutoka katika mapenzi yao. Kwa maana kuipenda na kuihifadhi dhambi, ni kumpenda na kumhifadhi mwasisi wake, yaani, adui yule wa hatari mno wa Kristo. Wanapotoa udhuru kwa ajili ya dhambi zao na kung'ang'ania tabia ile iliyopotoka, wanampa Shetani nafasi katika mapenzi yao, na kumsujudu. ----- RH, Agosti 12, 1884.

Mbingu yote inampenda mwanadamu na kutaka apate wokovu. Hilo ndilo kusudi kuu katika shughuli yote ya Mungu kwa mtu mmoja mmoja.... Ni jambo linalolishangaza mno jeshi lile la mbinguni kuona kwamba ni wachache mno wanaojali kuwekwa huru kutoka katika utumwa wa mivuto mibaya ya dhambi, wachache sana walio tayari kutumia nguvu zao zote kwa kuafikiana na Kristo katika kazi yake kuu ya ukombozi wao. Kama watu wangeonyeshwa mbele yao picha ya kazi zile anazozifanya yule mlaghai mkuu kwa kuwashikilia wanadamu katika uchungu mkali sana kama ule wa nyongo na kuwaweka katika utumwa ule wa dhambi, ni kwa bidii ilioje wangeyakataa kabisa matendo yale ya giza, ni kwa jinsi gani wangejilinda ili wasianguke majaribuni, wangekuwa waangalifu jinsi gani kuiona na kuiondoa kila kasoro inayoharibu sura ya Mungu ndani yao; kwa jinsi gani wangekaribia sana kando ya Yesu, na kwa jinsi gani dua zao za dhati zingepanda mbinguni ili wapate kutembea kwa amani, karibu zaidi, na kwa furaha na Mungu wao. ----- RH, Agosti 12, 1884.