IDARA YA VIJANA SINZA SDA

HISTORIA YA KANISA LA KRISTO KUPITIA UJUMBE WA BARUA SABA KWA MAKANISA SABA
MUHTASARI
Katika kitabu cha Ufunuo 2 - 3, tunasoma ujumbe wa Yesu Kristo kwa makanisa saba yaliyokuwako huko Asia ndogo yaani nchini Uturruki kwa sasa. Kila ujumbe kwa makanisa hayo saba una fundisho la kiunabii kwetu sisi juu ya uzoefu ambao watu wa Mungu wamepitia katika historia yote hadi sasa, na yale tunayozidi kupitia hadi wakati Yesu atakaporudi. Majina ya makanisa hayo saba ni miji saba iliyopatikana huko Asia ndogo ambayo ni Efeso, Smirna, Pergamo, Thiatira, Sardi, Filadelfia na Laodikia. Majina ya makanisa hayo saba huwakilisha ujumbe kuhusu hali na asili ya kanisa katika uzoefu wa vipindi saba tofauti katika historia ya Ukristo tangu kuanza kwa zama za ukristo mwaka 31 BK hadi hapo Yesu atakaporudi. 
1: EFESO: - ZAMA ZA MITUME (31 – 100 AD)
Hiki ni kipindi cha kanisa la Kristo katika zama za mitume, kilianza mwaka 31 BK – 100 BK.
Kiunabii Kanisa la Efeso huwakilisha kanisa la awali la Kikristo katika karne ya kwanza, ni kipindi cha muda wa kuanza kwa zama za Ukristo mnamo mwaka 31 BK wakati ambapo mashahidi wote wa kwanza walioshuhudia maisha na kazi ya Kristo walikwisha kupita. 
UZURI WA TABIA YA KANISA LA EFESO
Hali nzuri ya kanisa hili la kitume lilikuwa ni kanisa safi lenye nguvu kubwa ya kiroho kiasi kwamba halikuwa tayari kuvumilia uasi. Nguvu hiyo inahitajika hata sasa.
Utendaje wake ulisababisha kuenea kwa injili ulimwenguni kwa kiwango kikubwa kwa wakati huo.
ONYO KWA KANISA LA EFESO:
Yesu alitoa onyo kwa kanisa hili la awali la Kikristo kutokana na kupoteza upendo wake wa kwanza na mwamko juu ya Yesu na utume wake. Hivyo Yesu alikuwa akiwasihi warudi katika uzoefu wa upendo wa kwanza, wapate kutubu na kufanya matengenezo. Kwa maana pasipo upendo wa dhati  unaotubidiisha kwa Kristo ndani ya mioyo yetu dini yetu ni bure.
AHADI KWA KANISA LA EFESO:
Kwa kutii kwao onyo walilopewa, Yesu Kristo alitoa ahadi kwa kanisa la Efeso  kwa kupitia yeye wote wanaweza kuwa washindi na kuwa na uzima wa milele. 
2: SMIRNA: - ZAMA ZA MATESO (100 – 313 BK)
Hiki ni kipindi cha Kanisa la Kristo katika zama za mateso, kilianza mwaka 100 BK na kukoma mwaka 313 BK, wakati mtawala wa kirumi Mfalme Constatine alipotangaza uvumilivu wa kidini katika himaya yote. Kilikuwa kipindi cha mateso ya kuogofya na kuuwawa kwa watu waaminifu wa Mungu chini ya utawala wa Rumi ya kipagani. Ile nguvu ya Kiroho iliyokuwepo tangu kanisa la Efeso ilipelekea mateso makali kwa watu waaminifu wa Mungu. Mateso mabaya yalikuwa kwa muda wa miaka kumi ya mwisho (303-313 BK) chini ya utawala wa Rumi ya kipagani, kama ilivyoelezwa katika Ufunuo 2:10 kuwa ni "dhiki siku kumi"
UZURI WA TABIA YA KANISA LA SMIRNA
Hali nzuri ya kanisa hili la zama za mateso ni kuwa kanisa lililodumu katika ukuaji mkubwa wa kiroho licha ya mateso makali waliyopitia kutoka kwa utawala wa kirumi. Waliona ni afadhali kufa kuliko kumkana Yesu, walikuwa na matendo mema, bila kujali umaskini na dhiki waliyokuwa nayo.
ONYO KWA KANISA LA SMIRNA
Kutokana na kuwa waaminifu hata kufa pamoja na kuwa na mahusiano ya karibu sana na Yesu katika kuitetea imani. Hakukuwa na onyo lolote kwa kanisa la Smirna kwa maana Mungu alijua matendo yao na imani yao dhidi ya jaribu la mateso.
AHADI KWA KANISA LA SMIRNA
Bwana aliahidi kwa kanisa la Smirna kwamba, endapo watakuwa waaminifu hata kufa, atawapatia taji ya uzima (Ufunuo 2:10). "Yeye ashindaye hatapatikana na madhara ya mauti ya pili" 
3: PERGAMO: - ZAMA ZA MAAFIKIANO (313 – 538 BK)
Hiki ni kipindi cha zama za hatari kubwa kwa kanisa, Kanisa la Kristo kutokana na mateso kutoka kwa utawala wa kirumi, lilianza kufanya maafikiano hatimaye kuungwa mkono na serikali. Wakati Ukristo unakuwa maarufu na kusababisha mpasuko mkubwa ndani ya kanisa. Wachache walibaki waaminifu lakini wengi waliungana na serikali na kuweka misingi ya kuendeleza uasi wa Papa. Pergamo ilianza mwaka 313 BK-538 BK, ikijulikana kama "Kiti cha Shetani", kwasababu ndiyo kulikuwa makao makuu ya dini ya Romani Katoliki na Askofu wa Roma yaani Papa alifanywa kuwa mkuu wa makanisa yote. 
UZURI WA TABIA YA KANISA LA PERGAMO
Hali nzuri ya kanisa la Pergamo ni kuwa pamoja na maafikiano yaliyotokea bado kulikuwa na wengi wa watu ambao walidumu kuishika imani na kwenda kinyume na ukengeufu huu dhidi ya Ukristo. 
ONYO KWA KANISA LA PERGAMO
Bwana alilionya kanisa la Pergamo kwa kitendo cha kuruhusu mafundisho ya uongo kushamiri kanisani. Alilitaka kuwa makini dhidi ya shetani anayewafanya viongozi wake kuchanganya upagani na ukristo. Kwa maana kufanya hivyo kanisa liliingia katika hatia ya dhambi ya uasherati wa kiroho. Ezekiel 23:3. 
AHADI KWA KANISA LA PERGAMO
Yesu Kristo alitoa ahadi kwa kanisa la Pergamo kuwa wale waaminifu kwake, kamwe hawatahesabiwa hatia bali watapewa jiwe jeupe lililoandikwa jina jipya kuashiria usafi wao na kutokuwa na hatia, pamoja na uhusiano wao wa karibu na Yesu.
4: THIATIRA: - ZAMA ZA UASI (538 – 1560 BK)
Hiki ni kipindi cha kanisa la Kristo katika zama za giza, kilianza mwaka 538 BK hadi 1560 BK. Ni kipindi cha uasi wa kuogofya, mateso na kuuwawa kwa watu waaminifu wa Mungu. Hali iliyosababisha watu wa Mungu kukimbilia nyikani.
Maelewano kati ya kanisa na utawala wa kipagani ulisababisha kanisa kuwa na mapokeo ya kipagani hatimaye kusababisha Uasi wa kanisa. Walisahau kweli za Mungu, Biblia zilipigwa marufuku na wote waliokataa kuitambua mamlaka ya upapa waliteswa hadi kufa kama "wazushi". 
UZURI WA TABIA YA KANISA LA THIATIRA
Hali nzuri ya kanisa la Thiatira ni uwepo wa watu wachache walio na matendo mema, upendo, hali ya kuwahudumia wengine, subira na imani imara japokuwa walikabiliwa na mateso .
ONYO KWA KANISA LA THIATIRA
Yesu Kristo aliwaonya watu wa Thiatira waliopokea mafundisho ya kipagani na kuwaua watu wa Mungu, alikemea kutenda kwao kama Yezebeli, malkia aliyewauwa manabii wa Mungu na kuleta ibada ya sanamu kwa waisraeli . Bwana aliwasihi watu wa Pergamo  watubu na kuwa waangalifu na hila za shetani ili kuupata uzima wa milele.
AHADI KWA KANISA LA THIATIRA
Yesu Kristo alitoa ahadi kwa kanisa la Thiatira kuwa wasioshiriki katika uasi hataweka juu yao mzigo mwingine. Walicho nacho washike sana, hata atakapokuja kuwapa uzima wa milele, na kuwafanya watawala pamoja nae, kama wangeliishi maisha yote kulingana na Nuru waliyopewa.
5: SARDI:- ZAMA ZA MATENGENEZO (1560 – 1798 BK)
Hiki ni kipindi cha kanisa la Kristo katika zama muhimu za matengenezo ya Waprotestanti wakati ambapo watu wa Mungu walitikisa ulimwengu kwa Neno la Mungu. Kilianza mwaka 1560 hadi mwaka 1798 BK. Sardi maana yake “kile kilichosalia." kwa maana ni wale waaminifu waliosalia huko nyikani wakati wa zama za giza ndiyo waliongoza zama hizo za matengenezo.
Mwanzoni mwa matengenezo, makosa mengi ya zama za giza yaliwekwa wazi, Ukweli mwingi wa zamani uligundulika tena. Kama vile wokovu kwa njia ya imani katika Yesu Kristo, Biblia kama kanuni pekee ya imani na mafundisho, na Kristo kama mpatanishi pekee kati ya Mungu na mwanadamu. Hata hivyo, licha ya michango ya kishujaa ya viongozi binafsi wa kiprotestanti kama vile Martin Luther, John Calvin na Roger William, Msukumo wa matengenezo haukudumu, harakati zilipoa, walishindwa kuendeleza ukweli ambao viongozi wao waliugundua.
UZURI WA KANISA LA SARDI
Hali nzuri ya kanisa la Sardi ni kulikuwa na watu wengi ambao walikuwa na hamu ya neno la Mungu na hamu ya kupata uzoefu mahiri na Yesu Kristo.
ONYO KWA KANISA LA SARDI

Yesu alionya kanisa la Sardi kuacha tabia ya kudai kuwa hai kiroho na lenye matengenezo lakini limepoa. Kwa maana alilenga matengenezo yangaliendelea hadi injili safi itakaporejea tena.
AHADI KWA KANISA LA SARDI
Yesu Kristo alitoa ahadi kwa kanisa la Sardi kuwa washindi watavikwa "mavazi meupe" ambayo ni haki ya Kristo.
6: FILADELFIA: - ZAMA ZA UAMSHO (1798 BK – 1844 BK)
Hiki ni kipindi cha kanisa la Kristo katika zama za uamsho wa kiroho, kilianza mwaka 1798 BK hadi mwaka 1844 BK. Maeneo mengi duniani kote kulikuwa na uamsho mkuu wa kiroho, kuamka kwa injili nchini Uingereza na Uamsho mkuu katika Amerika yalifufua makanisa yaliyokuwepo na kuzidi kuwa imara hadi kuelekea uanzishwaji wa harakati za makanisa ya Baptisti na Methodisti. Misheni na vituo vya kujifunza biblia, vingi vilianzishwa na wamisionari wa kuzunguka maeneo mapya kama vile David Livingstone walijitokeza.
Kweli muhimu za biblia kama vile Sabato ya siku ya saba na kazi ya Yesu Kristo kama kuhani Mkuu kule patakatifu pa patakatifu zilivumbuliwa tena. Katika wakati huu Yesu Kristo alianza awamu ya mwisho ya huduma yake mbinguni mnamo mwaka 1844  kwa kuingia patakatifu pa patakatifu. Uamsho mkuu wa kiroho ulijulisha ulimwengu kwa kiwango kikubwa juu ya kurudi upesi kwa Yesu Kristo. 
UZURI WA KANISA LA FILADELFIA
Hali nzuri ya kanisa la Filadelfia ni walikuwa na nguvu ya kiroho, walishika na kutunza Neno la Kristo, hawakulikana jina la Yesu na walishika agizo lake la kuwa wavumilivu. Pamoja na kudharauliwa kutokana na kuamini juu ya unabii wa Biblia kuhusu Ujio wa pili wa Yesu Kristo. bado wamebaki na uvumilivu wakisubiri kurudi kwa Yesu Kristo.
AHADI KWA FILADELFIA
Yesu Kristo alitoa ahadi kwa kanisa la Filadelfia kuwa watalindwa zidi ya majaribu na wote watakaoshinda watafanywa kuwa "Nguzo katika hekalu la Mungu wangu" na kuwa na "Jina la Mungu".Wakiwa kama nguzo wao ni fahari pekee kutokana na msaada wao kwa kanisa la Kristo na wokovu wao ni wa hakika.
7: LAODIKIA: ZAMA ZA UVUGUVUGU (1844 – KUJA KWA KRISTO MARA YA PILI)
Hili ni kanisa la Mungu katika zama za uvuguvugu, kipindi chake kilianza miaka ya 1844, kimedumu hadi sasa, na kitaendelea kudumu hadi kuja kwa Yesu mara ya pili. Neno Laodikia linatokana na maneno mawili yanayomaanisha "watu" na "Hukumu." Hivyo kanisa la laodikia hujulikana kama kanisa katika kipindi cha kuanza hukumu kwa watu wote. 
Kipindi hiki kilianza wakati kanisa limeanza kupoteza bidii yake katika kazi ya utume, kimedumu hadi leo na kitaendelea hadi muda wa kurudi kwa Yesu Kristo. Hiki ndiyo kipindi tunachoishi leo, hakuna sifa yoyote nzuri kwa kanisa hili kama ilivyo kwa makanisa sita yaliyopita.
ONYO KWA KANISA LA LAODIKIA
Yesu anatoa karipio kwa kanisa la laodikia kutokuwa vuguvugu, analitaka kanisa la laodikia lichague kuwa moto au baridi badala ya kuwa vuguvugu. Kwa maana watu walio baridi unaweza kuhisi haja zao na kuwasaidia, na watu moto ni wale walio karibu na Bwana, lakini watu walio vuguvugu hawatambui wako mbali na Bwana kiasi gani. Wao ni vipofu juu ya hali zao za kweli za kiroho, hawajui kuwa wako uchi bila ya vazi la haki la Yesu Kristo. Na hii ndiyo hali ya kanisa la leo la Mungu yaani hali ya kanisa letu la SDA sasa.
Yesu anataka tujue yeye ndiyo chanzo cha utajiri wa kweli na ndiyo chanzo cha yote tunayosumbukia katika dunia hii, anataka watu wake waje kwake na kubadilisha hali ya kutokuamini kwao na ubinafsi wao ili kuwa dhahabu iliyotakaswa ya imani na upendo katika Kristo. 1 Petro 1:7; Wagalatia 5:6.
AHADI KWA KANISA LA LAODIKIA
Pamoja na ukweli kwamba hakuna jambo zuri toka kwa kanisa la laodikia ila tu ni maonyo dhidi yake, kanisa hili limepewa ahadi kuu kuliko makanisa yote yaliyopita. Yesu katika lugha ya picha anagonga katika malango ya mioyo yetu, na yeyote atakaye mkaribisha atafurahia uhusiano wake wa karibu na Yesu, atapokea nguvu kuwa mshindi na kupewa heshima kubwa ya kuketi pamoja nae katika kiti chake cha enzi. Luka 12:37; Yohana 14:23.
HITIMISHO
Katika ujumbe huu wa mwisho kwa kanisa la mwisho, Kristo anasihi watu wake wafanye toba kuwa waaminifu. Pia ni muhimu tuelewe kwamba uzoefu wa kanisa katika kipindi cha Efeso,
Smirna, na Pergamo utajirudia tena katika kanisa la mwisho la laodikia, kabla kuja kwa mara ya pili kwa Yesu Kristo, Vivyo hivyo uzoefu wa kanisa katika kipindi cha Thiatira utajirudia tena kwa kizazi cha mwisho. Hivyo ujumbe kwa kanisa la Filadelfia kuhusu kuwa na uvumilivu unapaswa kudumu katika akili zetu hadi mwisho wa wakati, na ni wale tu watakaopitia uzoefu huo wa kuvumilia ndiyo watavikwa taji. Je, umetoa maisha yako kwa Yesu Kristo? Kama bado, unaweza kufanya hivyo sasa kwa kusimama pamoja nasi ili tupate ombi la pamoja kwa ajili ya kutubu dhambi zetu, kushukuru maisha, kifo na ufufuo wa Yesu Kristo kwa ajili yetu na kumkubali Yesu Kristo kama Bwana na Mwokozi wa maisha yetu, akitupatia zawadi ya uzima wa milele.
OMBI....!!!

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Toa maoni hapa...