Jumapili, 6 Septemba 2015

SOMO LA ASUBUHI LEO

HEWA SAFI YA MAADILI 


Ili upate kwenda katika njia ya watu wema, Na kuyashika mapito ya wenye haki. (Mithali 2:20).

Ili kuwa na mwili wenye afya, ni lazima damu izungukayo katika mishipa iwe safi; ili ipate kuwa safi ni lazima ipate hewa safi na chakula safi. Matumizi ya chakula kisichofaa na uvutaji wa hewa chafu huleta ugonjwa ambao hujitokeza katika hali mbalimbali.

Usafi na ukamilifu wa maisha yetu ya kidini hutegemea sio tu juu ya kweli ile tunayoipokea, bali juu ya kundi lile tunaloongea nalo, na hewa ya maadili tunayoivuta. Imani, mabadiliko ya mwili na nguvu yake, kuwa na matumaini, kuwa na furaha, kuwa na mashaka na hofu, uvivu, upumbavu, wivu, kijicho, shuku, uchoyo, utukutu na kurudi nyuma, ni matokeo ya ushirikiano wa kirafiki tunaokuwa nao, kundi tunalotembea nalo, na hewa tunayovuta.

Kushiriki katika urafiki mbaya kutakuwa na matokeo yake maovu.... Biblia inaweza kusomwa na maombi kutolewa, bila kuwa na ongezeko lo lote la afya ya kiroho, wala kukua kiroho, kwa kadiri ilivyo mbaya hewa ile tunayovuta.... Uangalifu mkubwa sana ungetumika na waumini kujiweka wenyewe katika uhusiano wa karibu sana na Mungu, tena pamoja na wale waliofunzwa na Mungu. Ni jambo linaloumiza sana kuwaona wale waliouamini ukweli wa leo wakiingia katika wavu wa Shetani....

Tunapaza sauti zetu na kupiga kelele kwa kila muumini wetu aliye katika ukweli wa leo: Ukitaka kuwa na afya ya kiroho, angalia mapafu yako. Angalia chakula chako cha kiroho unachokula. Kuza upendo wako kwa jamii ya wale walio safi na wema, kama unataka kuwa na Kristo aliyeumbika ndani yako kama uzima wa roho yako. Afya ya roho yako hutegemea kuvuta hewa ile nzuri ya maadili. ----- Letter 1, 1882.

Kristo, Tabibu Mkuu, ameandika dawa ya kutumia kwa kila muumini. Yampasa kula chakula kile kitakachotolewa katika Neno la Mungu. Na imani ile itendayo kazi kwa upendo hutegemea sio tu juu ya chakula tulacho bali juu ya hewa tuvutayo. Tukifanya urafiki na wale walio waovu, tunavuta hewa iliyochafuliwa na malaria ya dhambi. Hakikisha kwamba kwa kufanya urafiki wako na wafuasi wa Yesu walio wapole na wanyenyekevu wa moyo, unavuta hewa safi, takatifu. ----- MS 60, 190l.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Toa maoni hapa...