CHUNGU CHA MAJARIBU MAKALI YATAKAYOLETA TAABU
Ole! maana siku ile ni kuu, hata hapana inayofanana nayo,
maana ni wakati wa taabu yake Yakobo; lakini ataokolewa nayo. Yeremia 30:7.
Njia inayoleta uhuru kutoka dhambini ni ile ya kuisulubisha
nafsi, na kupambana na nguvu zile za giza. Na asiwepo mtu ye yote wa kukatishwa
tamaa kwa sababu ya maonjo makali watakayokutana nayo katika kipindi kile cha
wakati wa taabu ya Yakobo ambacho kiko mbele yao. Wanapaswa kufanya kazi kwa
bidii, kwa wasiwasi, si kwa ajili ya wakati ule, bali kwa leo hii. Tunachotaka
ni kupata maarifa ya ile kweli kama ilivyo katika Kristo hivi sasa, na kuwa na
uzoefu sasa kila mmoja wa kwake [wa maisha yale ya ushindi dhidi ya kila
dhambi]. Katika saa hizi za thamani za kufungia mlango wa rehema, tunapaswa
kuwa na uzoefu huo wenye kina na ulio hai. Kwa njia hiyo, tutajenga tabia zile
zitakazotuhakikishia kuokolewa kwetu katika wakati ule wa taabu.
Wakati wa taabu ni chungu cha majaribu makali
ambacho kitazidhihirisha [ndani ya watu wake] tabia zile zinazofanana na ile ya
Kristo. Kimekusudiwa kuwaongoza watu wa Mungu wafikie mahali pa kumkataa
Shetani na majaribu yake. Pambano lile la mwisho litamfunua kwao Shetani kwa
tabia yake halisi, yaani, ile ya mtawala katili anayetumia mabavu, nalo
litawafanyia mambo yale ambayo hakuna kitu kingine cho chote ambacho kingeweza
kuyafanya, yaani, kumng'oa kabisa [Shetani] kutoka katika mapenzi yao. Kwa
maana kuipenda na kuihifadhi dhambi, ni kumpenda na kumhifadhi mwasisi wake,
yaani, adui yule wa hatari mno wa Kristo. Wanapotoa udhuru kwa ajili ya dhambi
zao na kung'ang'ania tabia ile iliyopotoka, wanampa Shetani nafasi katika
mapenzi yao, na kumsujudu. ----- RH, Agosti 12, 1884.
Mbingu yote inampenda mwanadamu na kutaka
apate wokovu. Hilo ndilo kusudi kuu katika shughuli yote ya Mungu kwa mtu mmoja
mmoja.... Ni jambo linalolishangaza mno jeshi lile la mbinguni kuona kwamba ni
wachache mno wanaojali kuwekwa huru kutoka katika utumwa wa mivuto mibaya ya
dhambi, wachache sana walio tayari kutumia nguvu zao zote kwa kuafikiana na
Kristo katika kazi yake kuu ya ukombozi wao. Kama watu wangeonyeshwa mbele yao
picha ya kazi zile anazozifanya yule mlaghai mkuu kwa kuwashikilia wanadamu
katika uchungu mkali sana kama ule wa nyongo na kuwaweka katika utumwa ule wa
dhambi, ni kwa bidii ilioje wangeyakataa kabisa matendo yale ya giza, ni kwa
jinsi gani wangejilinda ili wasianguke majaribuni, wangekuwa waangalifu jinsi
gani kuiona na kuiondoa kila kasoro inayoharibu sura ya Mungu ndani yao; kwa
jinsi gani wangekaribia sana kando ya Yesu, na kwa jinsi gani dua zao za dhati
zingepanda mbinguni ili wapate kutembea kwa amani, karibu zaidi, na kwa furaha
na Mungu wao. ----- RH, Agosti 12, 1884.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Toa maoni hapa...