Jumatano, 21 Oktoba 2015

SOMO LA ASUBUHI LEO

JE, NINAMWAKILISHA BWANA WANGU IPASAVYO?


Ninyi ni mashahidi wangu, asema BWANA, na mtumishi niliyemchagua.( Isaya 43:10).

Iwapo waumini wanafanya urafiki na wale wasioamini kwa kusudi la kuwaleta kwa Kristo, basi, watakuwa mashahidi wake Kristo, na baada ya kutekeleza utume wao huo, watajitenga ili kuvuta hewa safi na takatifu. Wataweza kumkaribia Mungu, na kupeleka dua zao juu kwa Kristo kwa niaba ya rafiki zao na wale wanaoshirikiana nao, wakijua kwamba anaweza kuwaokoa kabisa wale wote wamjiao Mungu kwa yeye.

Unapokuwa katika jamii ya wasioamini, kumbuka daima kwamba kwa tabia yako wewe u mwakilishi wake Yesu Kristo, usiruhusu maneno ya kipuuzi, na yale yasiyo na maana, yaani, maongezi ya kipuuzi, kutoka kinywani mwako. Zingatia thamani ya roho ya mtu, nawe kumbuka kwamba ni haki yako na wajibu wako kwa kila njia inayowezekana kuwa mtenda kazi pamoja na Mungu. Usijishushe hadhi yako ili upate kuwa sawa na wale wasioamini, na kucheka na kusema maneno yasiyo na maana kama wao wanavyofanya. Kwa kufanya hivyo... unajiweka katika hali moja na mwenye dhambi yule. Mwenendo kama huo utakufanya uwe kikwazo katika njia ya wenye dhambi....


Roho Mtakatifu anapougusa moyo wetu, ingetupasa kushirikiana na mvuto wake unaozibadilisha tabia zetu, nasi tutakuwa na hamu ya kupata mambo yale yaliyo bora, ufahamu safi wa ile kweli, upole, kuwa wepesi kufundishwa, tena tutaweza kuitekeleza kazi yetu kwa unyenyekevu. Hiyo ndiyo njia ambayo kwayo wewe utaweza kumjua vema Mungu, na kumjua Mungu ni haki ya Mkristo. Hapo ndipo unaweza kufanya kazi kwa ajili ya wale wasioongoka, na jamii ya wasioamini haitakuletea madhara yo yote, kwa kuwa maisha yako yatakuwa yamefichwa pamoja na Kristo katika Mungu, nawe utatafuta urafiki kwa wale walio nje ya Kristo kwa madhumuni ya kuwaongoa wapate kumtumikia yeye. Umoja wako na Mungu hukufanya uwe na nguvu kiroho, ili upate kustahimili mivuto yo yote mibaya inayoweza kutoka kwao....

Hakikisha kwamba wewe mwenyewe unajiweka katika njia ile ya nuru, na kwa matendo yako unakuwa mfuasi wake yeye aliyekwenda huku na huku "akitenda mema." ----- Letter 51, 1894.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Toa maoni hapa...