CHUNGA HATUA YAKO!
Ulisawazishe pito la
mguu wako, Na njia zako zote zithibitike. Mithali 4:26.
"Mkaifanyie
miguu yenu njia za kunyoka," asema mtume, "ili kitu kilicho kiwete
kisipotoshwe." Waebrania 12:13. Njia ile inayokwenda mbali na Mungu,
yaani, mbali na kanuni yake ya haki, takatifu, na kamilifu [Amri Kumi],
sikuzote imepotoka na ni ya hatari. Hata hivyo... wengi wamekuwa wakienda
katika njia hiyo ya uasi. Katika mifano mingi [inayofahamika], hawakuanza
vizuri katika utoto na ujana wao, nao wamezifuata njia hizo potofu katika
safari yao yote. Sio tu kwamba wao wenyewe wamekosa kwa kuiacha njia ile ya
kweli, bali kwa mvuto wa mfano wao wengine vile vile wamepotoshwa kutoka katika
njia ile dhahiri iliyonyoka, nao wamefanya makosa ya kufisha....
Sikuzote huwa hatuitambui
nguvu ya kielelezo. Tunakutana na wengine. Tunakutana na watu wanaotenda
makosa, yaani, wanaotenda dhambi kwa njia mbalimbali; huenda wakawa ni watu
wasiokubalika, wepesi kutenda, wenye harara na watumiaji wa mabavu.
Tunaposhughulika na watu kama hao yatupasa kuwa wavumilivu, wastahimilivu,
wapole, na waungwana. Shetani anafanya kazi yake kupitia kwao kuleta chokochoko
kwetu na kutuhangaisha, ili tusipate nafasi ya kuonyesha tabia nzuri ya
kupendeza. Kuna maonjo na matatizo kwa ajili yetu tunayopaswa kupambana nayo;
kwa maana sisi tumo katika ulimwengu wa masumbufu, wasiwasi, na kukata tamaa.
Lakini maudhi hayo yanayoendelea daima hayana budi kushughulikiwa katika roho
ya Kristo. Kwa njia ya neema yake tunaweza kuinuka na kuwa washindi wa mazingira
yetu, na kuzihifadhi roho zetu katika hali ya ukimya na utulivu katikati ya
mahangaiko na masumbufu ya maisha ya kila siku. Kwa njia hiyo, sisi tutaweza
kumwakilisha Kristo kwa ulimwengu....
Kujitoa wakf kwa
Mungu ni lazima liwe jambo lililo hai, linalofanywa kwa vitendo; sio nadharia
tu ya kuzungumza habari zake, bali kanuni iliyosukwa pamoja na maisha yetu.
Tungeiacha nuru yetu iangaze mbele ya wengine ili, wanapoyaona matendo yetu
mema, wapate kumtukuza Baba yetu aliye Mbinguni. Yatupasa kuzitangaza sifa zake
yeye aliyetuita tutoke gizani tukaingie katika nuru yake ya ajabu. Iwapo nuru
ya mbinguni imo ndani ya moyo wetu, basi, itaakisiwa kwa wote wanaotuzunguka.
Natamani wote wangeweza kuliona somo hili la maana katika nuru yake halisi.
Hapo ndipo pasingalikuwapo na hali hii ya kutojali kutumia maneno na kutenda
matendo yasiyofaa, wala kuishi maisha haya ya ovyo, ya kizembe, yasiyokuwa ya
dini. ----- ST, Jan. 1, 1885.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Toa maoni hapa...