SHULE YA AKILI NA MAADILI
Nao wauimba wimbo wa Musa, mtumwa wa Mungu, na
wimbo wa Mwana-Kondoo, wakisema, Ni makuu, na ya ajabu, matendo yako, Ee Bwana
Mungu Mwenyezi; Ni za haki, na za kweli, njia zako, Ee Mfalme wa mataifa. (Ufunuo 15:3.)
Mwasisi Mkuu ameumba na kuzitengeneza mandhari
mbalimbali katika maumbile [ulimwengu huu] ili zipate kuwa na maana kubwa
katika tabia ya mwanadamu kiakili na kimaadili. Hizo zinatakiwa ziwe shule ya
Mungu ya kuikuza akili na maadili. Hapo ndipo akili inaweza kuwa na nyanja pana
sana ya utafiti katika maonyesho hayo ya matendo makuu ya Mungu wa milele.
Miamba ni miongoni mwa vitu vya thamani ulimwenguni, ikiwa na hazina za hekima
na maarifa. Katika miamba na milima hiyo umeandikwa ukweli kwamba hakika Mungu
aliwaangamiza kwa Gharika wale waovu juu ya uso wa nchi hii. ----- MS 73, 1886.
Watu wale walijifikiria wenyewe kwamba
walikuwa na hekima kuliko Mungu, na hekima ya kupindukia hata wasitake kutii...
sheria na amri zake Yehova. Utajiri wa dunia hii aliowapa Mungu haukuwafanya
kutii, bali kuasi, kwa sababu walivitumia vibaya vipawa vizuri vilivyotoka
mbinguni, na kuifanya mibaraka ile waliyopewa na Mungu kuwa vitu vya kuwatenga
mbali na Mungu. Na kwa kuwa walikuwa na tabia kama ile ya Shetani, badala ya
ile ya Mungu, Bwana alituma maji ya Gharika juu ya ulimwengu ule wa zamani.
----- MS 62, 1886.
Mungu amejaa upendo, naye ni
mwingi wa rehema; lakini kwa vyo vyote vile hataweza kuwaachilia [pasipo kuwapa
adhabu] wale wasioujali wokovu wake mkuu aliowapa. Wakazi wale walioishi kwa
miaka mingi sana kabla ya Gharika wakafagiliwa mbali kutoka juu ya uso wa nchi
hii kwa sababu waliitangua sheria ya Mungu. Mungu hataleta tena maji kutoka
katika mbingu za juu na chini ya nchi hii kama silaha zake za kutumia katika
maangamizi ya ulimwengu huu; bali kisasi kinachokuja kitakapomwagwa juu ya wale
wanaoyadharau mamlaka yake, [waovu] wataangamizwa kwa moto uliofichwa chini
kabisa ya dunia hii, utakaochochewa sana na kufanya kazi yake kwa mioto ile
itakayotoka mbinguni juu. Baada ya tukio hilo ndipo kutoka katika nchi hii
iliyotakaswa utaimbwa wimbo huu wa sifa: "Baraka na heshima na utukufu na
uweza una yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, na yeye Mwana-Kondoo, hata milele
na milele." Ufunuo 5:13. "Ni makuu, na ya ajabu, matendo yako, Ee
Bwana Mungu Mwenyezi; Ni za haki na za kweli, njia zako, Ee Mfalme wa mataifa
[watakatifu]." Na kila mmoja aliyeifanya hazina ile ya mbinguni kuchukua
nafasi ya kwanza katika mawazo yake, atajiunga kuimba wimbo huo mkuu wa
ushindi.- RH, Feb. 24, 1885.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Toa maoni hapa...