Jumamosi, 5 Septemba 2015

SOMO LA ASUBUHI LEO

HARUFU NZURI KATIKA KAZI YETU YA MAISHA


Na mavazi, ya nini kuyasumbukia? Fikirini maua ya mashamba, jinsi yameavyo; hayafanyi kazi, wala hayasokoti, nami nawaambia, ya kwamba hata Sulemani katika fahari yake yote hakuvikwa vizuri kama mojawapo la hayo. Mathayo 6:28,29.

Msanii wetu Mkuu anayageuza mawazo yetu kuelekea kwenye maua ya mashamba yasiyokuwa na roho, akituonyesha rangi zake nzuri na aina mbalimbali za rangi ambazo ua moja linaweza kuwa nazo. Kwa njia hiyo, Mungu ametufunulia ustadi na utunzaji wake. Hivyo ndivyo ambavyo angelionyesha pendo lake alilo nalo kwa kila mwanadamu. ----- 5BC 1086.

Bwana Muumbaji wetu anatumia uangalifu mkubwa, hekima, na muda wake juu ya ua dogo sana kama vile anavyotumia juu ya mambo yale makuu anayoyaumba. Katika maua yaliyo madogo sana huonekana uzuri na ukamilifu ambao hakuna sanaa ya kibinadamu yo yote iwezayo kuufuatisha. Pambo lile lenye mistari-mistari inayovutia sana la ua waridi ambalo limetiwa rangi, na nyota zile zilizoko mbinguni, huionyesha ile kalamu iliyochora ya Msanii huyo Mkuu.

Maua mazuri sana... huonyesha faida ya kukua na kupevuka kwa akili na mwili wa kibinadamu kutokana na mafunzo au uzoefu wa kutenda kazi. Yanatufundisha kwamba ni haki yetu kujiendeleza. Mungu anatutaka sisi kuleta harufu nzuri katika kazi yetu ya maisha. Tunatakiwa kuwa mimea yake Bwana, kumtumikia kwa njia yo yote anayopenda yeye. Hebu na tufanye kila linalowezekana kuzifanya tabia zetu ziweze kupendeza.... Uangalifu mkuu unapaswa kutolewa kwa mimea hiyo myororo. Chipukizi ambazo hazina faida lazima ziondolewe. Sehemu zilizochubuliwa sharti zifungwe kwa uangalifu. Kwa hiyo wale walio dhaifu katika imani wanapaswa kuwa na matunzo ya kuwalea. Yatupasa kuwashirikisha wale walio dhaifu katika makusudi yetu yenye nguvu katika bustani ya Bwana, tukiwapa msaada unaohitajika. ----- MS 47, 1898.

Kutokana na aina mbalimbali za mimea ambazo hazina mwisho, tunaweza kujifunza fundisho la maana. Chipukizi zote za maua hazifanani kwa umbo wala kwa rangi. Nyingine zina nguvu za kuponya magonjwa. Nyingine zinatoa harufu nzuri sikuzote. Kuna wale wanaojiita Wakristo ambao hudhani kwamba ni jukumu lao kumfanya kila Mkristo kuwa kama wao wenyewe walivyo. Huo ni mpango wa mwanadamu, sio mpango wa Mungu. Katika kanisa la Mungu kuna nafasi kwa tabia mbalimbali kama vile maua yalivyo katika bustani. Katika bustani yake ya kiroho kuna maua mengi ya aina mbalimbali. ----- Letter 95, 1902.

Bwana ndiye anayeyatunza maua. Anayapa uzuri wake na harufu nzuri. Je! hatazidi sana kutupa sisi harufu nzuri ya tabia iliyo changamfu? ----- Letter 153, 1902. 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Toa maoni hapa...