Jumamosi, 25 Julai 2015

IBADA YA SABATO YA LEO, Julai 25, 2015: - "MUNGU AMETUCHAGUA TUFANYWE WATOTO WAKE" - hubiri kutoka kwa Mchungaji Amos Lutebekela

WIMBO: Namba  142- NASIKIA MWITO

FUNGU KUU:,"kama vile alivyotuchagua katika yeye kabla ya kuwekwa misingi ya ulimwengu, ili tuwe watakatifu, watu wasio na hatia mbele zake katika pendo. 5Kwa kuwa alitangulia kutuchagua, ili tufanywe wanawe kwa njia ya Yesu Kristo, sawasawa na uradhi wa mapenzi yake." ( Waefeso 1:4 - 5)
UFAFANUZI:
Ni Mungu anayetuchagua na kutupatia uwezo wa kufanya kila jambo, hata tendo hili la kuingia kanisani katika sabato ya leo ni Mungu ndiyo amechagua, na hili hutokea mara tu pale tunapokubali uchaguzi huu uliotoka kwa Mungu yaani kuchaguliwa kuwa watoto wa Mungu.
Kwa mfano hata katika hali ya kibinadamu kuna mambo hatuwezi kuchagua sisi kama sisi mojawapo ni, kuchagua uzaliwe na nani , hakuna mtu yeyote anayeweza kuchagua azaliwe na nani. 
Jambo zuri katika somo la leo ni kwamba Mungu ametoa ahadi ya pekee kwetu kwamba kila mmoja wetu amechaguliwa kuwa mwana wa Mungu (Yohana 1:12-13)
Pia ni vema kuelewa habari ya kuwa mtoto wa Mungu haianzi kwa njia ubatizo bali inaanza mara tu baada ya mtu kumpokea Kristo kama Bwana na Mwokozi wake.
Hivyo basi inawezekana ukawa mwana wa  Mungu kabla hata ya kubatizwa, na unaweza kubatizwa lakini usiwe mwana wa Mungu kwa maana ya kuishika ile kweli yote.
Mtu anapokuwa mtoto wa Mungu kwa uwezo wa Roho Mtakatifu anaanza kupandikizwa tabia ya Mungu, hivyo unapokubali huu uchaguzi wa Mungu kwamba wewe ni mtoto wa Mungu basi mtindo wa maisha yako utatenda kwa kudhihirisha tabia ya Mungu.
WITO
Ili kushinda majaribu ya shetani ni lazima kila mmoja wetu akubali kuchaguliwa kuwa mtoto wa Mungu kwa njia ya Yesu Kristo yaani kuwa na ushirika nae kwa kumfanya awe Bwana na Mwokozi wa Maisha yako. Na kwa neema ya Mungu wale wote wanaokubali kuwa watoto wa Mungu zawadi wanazopewa moja kwa moja kutoka kwa Mungu ni
  1. Nguvu ya kushinda dhambi
  2. Kumkiri Yesu mbele za watu bila aibu
  3. Ujasiri wa kutangaza habari za Yesu kwa watu
Lazima tuelewe jukumu letu si kuomba Mungu atuchague tuwe watoto wake kwa maana aliisha tuchagua tangu hapo mwanzo, bali jukumu letu ni kukubali huo uchaguzi wa kuchaguliwa naye.
Hebu tujitoe wakifu mbele za Mungu ili kuachana na dhambi, na tukubali kujikana nafsi kwa kujitoa kikamilifu mbele za Mungu. Usiangalie nani anakuangalia bali muangalie Yesu pekee nawe utapata wokovu.

Bwana Yesu Kristo awabariki zaidi na zaidi  Amina!!!




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Toa maoni hapa...