VIUMBE VYA ASILI HUMTANGAZA MUNGU
Nimezikumbuka siku
za kale, Nimeyatafakari matendo yako yote, Naziwaza kazi za mikono yako.
Nakunyoshea mikono yangu; Nafsi yangu inakuonea kiu kama nchi kame. (Zaburi
143:5,6.)
Tumeiangalia milima mirefu sana yenye matuta ya mkingamo
katika uzuri wake mkuu, pamoja na buruji zake za miamba zinazofanana na nyumba
kubwa za zamani zenye boma [ngome]. Milima hiyo hututangazia sisi ghadhabu ya
Mungu iangamizayo ili apate kuithibitisha sheria yake iliyovunjwa; kwa maana
[milima hiyo] iliinuliwa juu kwa tetemeko lililoitikisa sana nchi wakati ule wa
Gharika. Ni kama mawimbi yenye nguvu nyingi sana yaliyosimama wakati
yaliposikia sauti ya Mungu ----- mawimbi yaliyogandishwa, yaliyozuiwa katika
kiburi chake kikubwa sana na kuwa mawimbi makubwa. Milima hiyo mirefu sana ni
yake Mungu; anakaa juu ya ngome za miamba yake iliyo imara. Utajiri unaotokana
na migodi yake ni wake pia, na hivyo ndivyo vilivyo mali yake vilindi vile
virefu vya nchi.
Ukitaka kuona
ushahidi kwamba Mungu yuko, angalia pande zote po pote bahati yako inapoweza
kukuangukia. Anazungumza na fahamu zako na kuugusa moyo wako kwa njia ya kazi
zake alizoziumba. Hebu moyo wako na uzipokee picha hizo, ndipo viumbe vya asili
vitakuwa kitabu kilichofunguliwa kwako, na vitakufundisha kweli ya Mungu kwa
njia ya vitu vya kawaida unavyovifahamu. Miti mirefu sana haitaangaliwa kwa
moyo usiojali. Kila ua linalochipua, kila jani lenye mishipa yake myororo,
litashuhudia ustadi usio na kifani wa yule Msanii Mkuu sana. Miamba mikubwa
sana na milima mirefu sana inayoinuka kule mbali si matokeo ya nasibu.
Inatangaza kwa lugha ya kimya inayoshawishi habari za yule Mmoja anayekaa juu
ya kiti cha enzi cha malimwengu, yule aliye juu na mwenye kutukuzwa. "Kazi
zake zote zajulikana kwa Mungu tangu mwanzo wa ulimwengu." Mipango yake
yote ni mikamilifu. Ni kicho na heshima ilioje jina lake lingeweza kuamsha
ndani yetu!...
Mungu mwenyewe ndiye Mwamba wetu
wa Kale, kimbilio la watu wake, kificho mbali na dhoruba, kivuli jua kali
linapounguza. Ametupatia ahadi zake, ambazo ni imara zaidi na madhubuti kuliko
miinuko hiyo ya miamba, ni milima ile ya milele. Milima itatoweka, na vilima
vitaondolewa; bali fadhili zake hazitaondoshwa, wala agano lake la amani
halitaondolewa kwa wale ambao kwa imani wanamfanya yeye kuwa tegemeo lao. Iwapo
tungeweza kumtazamia Mungu kutupa msaada wake kwa uthabiti kama ule wa milima
hiyo kame yenye miamba, inayozielekea mbingu zilizo juu yake, basi, tusingeweza
kuondolewa kamwe katika imani yetu kwake wala katika utii wetu kwa sheria yake
takatifu. ---RH, Feb. 24, 1885.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni
Toa maoni hapa...