Alhamisi, 10 Septemba 2015

SOMO LA ASUBUHI LEO

RAFIKI KWA WALE WASIOKUWA NA RAFIKI 


Marhamu na manukato huufurahisha moyo; Kadhalika utamu wa rafiki ya mtu utokao katika kusudi la moyo wake. Mithali 27:9.

Ingetupasa sisi kuwa na upendo wa Kristo moyoni mwetu kwa kiwango kile ambacho kuwapenda wengine kutakuwa kwa haki na unyofu. Mapenzi yetu yangekuwa na upeo mpana, wala yasingewekwa tu kwa wachache wanaojipendekeza kwetu kwa kutuambia siri zao muhimu. Mwelekeo wa urafiki kama huo ni kutufanya tuwasahau wale walio na hitaji kubwa la kupendwa kuliko wale ambao mawazo yetu yanaelekea kwao.

Tusingeifanya duara ya marafiki zetu kuwa ndogo kwa kuwaingiza wale walio wachache sana tunaowapenda sana kwa sababu wanatubembeleza na kujipendekeza kwetu kwa madai yao ya kutupenda. Kuwapendelea hao wachache kwa kuwapa na kupokea usikivu, hakuleti manufaa ya hali ile ya juu kwa wale ambao wangependa kumtumikia Mungu. Mmoja anapata nguvu yake kutoka kwa mwingine, kisha sifa, kujipendekeza na upendo anapokea kwa mwingine, mambo hayo huchukua nafasi ile ambayo ingejazwa na neema ya Mungu, na kwa njia hiyo marafiki wa kibinadamu huyaondoa mapenzi yetu kutoka kwa Kristo.... Wasiri wa kibinadamu, marafiki wa kibinadamu, huchukua upendo wote na matumaini yote ambayo angestahili kupewa Mungu peke yake....

Badala ya wewe mwenyewe kutaka upendwe sana, au kujipendekeza kwa mtu mmoja ambaye huenda anaheshimiwa sana, angalia iwapo hakuna mtoto maskini ye yote ambaye hapendwi, ambaye hakuna wema wo wote maalum unaoonyeshwa kwake, nawe mfanye huyo kuwa lengo la usikivu wako usio na ubinafsi. Wale ambao wanavutia hasa hawatakosa marafiki; ambapo wale ambao hawapendezi kabisa kwa mwonekano wao, ambao ni waoga na wagumu kufanya urafiki nao, wanaweza kuwa na sifa nzuri za tabia, hao nao wamenunuliwa kwa damu yake Kristo. ----- YI, Mei 25, 1893. 

Hisia zako za kuwa na wasiwasi, kutamani kurudi nyumbani, au upweke huenda zikawa kwa faida yako. Baba yako aliye mbinguni ana maana ya kukufundisha wewe ili uweze kupata ndani yake urafiki na upendo na faraja ambayo itakidhi matumaini na tamaa zako za dhati.... Usalama na furaha yako ya pekee ni katika kumfanya Kristo kuwa mshauri wako wa kudumu. Unaweza kuwa na furaha ndani yake kama hujawahi kuwa na rafiki mwingine ye yote katika ulimwengu huu mpana. ----- Letter 2b, 1874

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Toa maoni hapa...