Ijumaa, 3 Julai 2015

Neno la leo 

Ijumaa, Julai 3, 2015

Ufunuo 7
Kupigwa mhuri kwa watu 144,000 wa Israeli
1Baada ya hayo nikawaona malaika wanne wamesimama katika pembe nne za dunia, wakishika pepo nne za dunia ili upepo usivume hata kidogo: Wala katika nchi, wala baharini, wala kwenye miti. 2Kisha, nikamwona malaika mwingine akipanda juu kutoka mashariki, akiwa na mhuri wa Mungu aliye hai. Akapaza sauti na kuwaambia hao malaika wanne waliokabidhiwa jukumu la kuiharibu nchi na bahari, 3“Msiharibu nchi, wala bahari, wala miti, mpaka tutakapokwisha wapiga mhuri watumishi wa Mungu wetu katika paji la uso.” 4Kisha, nikasikia idadi ya hao waliopigwa mhuri: Watu 144,000 wa makabila yote ya watu wa Israeli. 5Kabila la Yuda, watu 12,000; kabila la Reubeni, 12,000; kabila la Gadi, 12,000; 6kabila la Asheri, 12,000; kabila la Naftali, 12,000; kabila la Manase, 12,000; 7kabila la Simeoni, 12,000; kabila la Lawi, 12,000; kabila la Isakari, 12,000; 8kabila la Zebuluni, 12,000; kabila la Yosefu, 12,000; na kabila la Benyamini, 12,000.
Umati wa watu wa kila taifa
9Kisha, nikatazama, nikaona umati mkubwa wa watu wasiohesabika: Watu wa kila taifa, ukoo, jamaa na lugha. Nao walikuwa wamesimama mbele ya kiti cha enzi na mbele ya Mwanakondoo, wamevaa mavazi meupe na kushika matawi ya mitende mikononi mwao. 10Wakapaza sauti: “Ukombozi wetu watoka kwa Mungu wetu aketiye juu ya kiti cha enzi, na kutoka kwa Mwanakondoo!” 11Malaika wote wakasimama kukizunguka kiti cha enzi, wazee na wale viumbe hai wanne. Wakaanguka kifudifudi mbele ya kiti cha enzi, wakamwabudu Mungu, 12wakisema, “Amina! Sifa, utukufu, hekima, shukrani, heshima, uwezo na nguvu viwe kwa Mungu wetu, milele na milele! Amina!”
13Mmoja wa hao wazee akaniuliza, “Hawa waliovaa mavazi meupe ni watu gani? Na wametoka wapi?” 14Nami nikamjibu, “Mheshimiwa, wewe wajua!” Naye akaniambia, “Hawa ni wale waliopita salama katika ule udhalimu mkuu. Waliyaosha mavazi yao katika damu ya Mwanakondoo, yakawa meupe kabisa. 15Ndiyo maana wako mbele ya kiti cha enzi cha Mungu. Humtumikia Mungu mchana na usiku katika hekalu lake; naye aketiye juu ya kiti cha enzi atatandaza hema lake juu yao kuwalinda. 16Hawataona tena njaa wala kiu; jua wala joto kali halitawachoma tena,17kwa sababu Mwanakondoo aliye katikati ya kiti cha enzi atakuwa mchungaji wao, naye atawaongoza kwenye chemchemi za maji ya uhai. Naye Mungu atayafuta machozi yote machoni mwao.”
Ufunuo 8
Mhuri wa saba
1Na Mwanakondoo alipouvunja mhuri wa saba, kukawa kimya mbinguni kwa muda wa nusu saa. 2Kisha, nikawaona wale malaika saba wanaosimama mbele ya Mungu wamepewa tarumbeta saba.
3Malaika mwingine akafika, anachukua chetezo cha dhahabu, akasimama mbele ya madhabahu ya kufukizia ubani. Naye akapewa ubani mwingi autoe sadaka pamoja na sala za watu wote wa Mungu juu ya madhabahu ya dhahabu iliyo mbele ya kiti cha enzi. 4Moshi wa ubani ukapanda juu, pamoja na sala za watu wa Mungu kutoka mikononi mwake huyo malaika aliyekuwa mbele ya Mungu.5Kisha, malaika akakichukua hicho chetezo, akakijaza moto wa madhabahuni, akakitupa duniani. Kukawa na ngurumo, sauti, umeme na tetemeko la ardhi.
Tarumbeta
6Kisha, wale malaika saba wenye tarumbeta saba wakajiweka tayari kupiga mbiu ya mgambo.
7Malaika wa kwanza akapiga tarumbeta yake. Mchanganyiko wa mvua ya mawe na moto pamoja na damu ukamwagwa juu ya nchi. Theluthi moja ya nchi ikaungua, theluthi moja ya miti ikaungua na majani yote mabichi yakaungua.
8Kisha malaika wa pili akapiga tarumbeta yake. Na kitu kama mlima mkubwa unaowaka moto kikatupwa baharini. Theluthi moja ya bahari ikawa damu, 9theluthi moja ya viumbe vya baharini vikafa, na theluthi moja ya meli zikaharibiwa.
10Kisha, malaika wa tatu akapiga tarumbeta yake. Na nyota kubwa ikiwaka kama bonge la moto ikaanguka kutoka mbinguni na kutua juu ya theluthi moja ya mito na chemchemi za maji. 11(Nyota hiyo inaitwa “Uchungu.”) Basi, theluthi moja ya maji yakawa machungu; watu wengi wakafa kutokana na maji hayo, kwa sababu yaligeuka kuwa machungu.
12Kisha, malaika wa nne akapiga tarumbeta yake. Ndipo theluthi moja ya jua, ya mwezi na ya nyota ikapata pigo; hata mwangaza ukapoteza theluthi moja ya mng'ao wake. Theluthi moja ya mchana ikakosa mwanga, hali kadhalika na theluthi moja ya usiku.
13Kisha, nikatazama, nikasikia tai akiruka juu kabisa angani, anasema kwa sauti kubwa, “Ole, ole, ole kwa wanaoishi duniani wakati malaika watatu waliobaki watakapopiga tarumbeta zao!”

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Toa maoni hapa...