Jumanne, 14 Julai 2015

KESHA LA ASUBUHI: HIVI NI KWELI TUNAJITOLEA MHANGA? Jumanne, Julai 14, 2015

Washangilie,wakufurahie, Wote wakutafutao.

Waupendao wokovu wako waseme daima, Atukuzwe BWANA. Zaburi 40:16. Wengi wanasema juu ya maisha ya Mkristo kuwa yanatuondolea anasa na raha za dunia.

Mimi nasema hayaondoi kitu chochote kinachofaa kukitunza. Je, kuna mashaka, umaskini, na dhiki anayopata Mkristo? Ndiyo, jambo hilo linatazamiwa katika maisha haya.
Lakini mwenye dhambi tunayesema anafurahia anasa za ulimwengu huu, je! yu huru mbali na mabaya hayo yanayopatikana katika maisha haya? Je! hatuwaoni mara kwa mara wakiwa katika mashaka makubwa na taabu?...  

Wakati mwingine Wakristo wanadhani ya kwamba wanao wakati mgumu na ya kwamba ni kujidhalilisha wenyewe kuishikilia kweli hii isiyopendwa na watu wengi na kukiri kuwa wao ni wafuasi wake Kristo, kwamba kwao njia huonekana  kuwa ngumu na kwamba wanayo mambo mengi yanayowataka kujitolea mhanga, ambapo ukweli ni kwamba hawajitoi mhanga hata kidogo. 

Iwapo wao wameingizwa kweli katika familia ya Mungu, je! wametoa kafara gani?Kumfuata kwao Kristo kunaweza kuwa kumevunja urafiki fulani pamoja na ndugu zao waipendao dunia hii, lakini, basi, angalia walichobadilishana----- majina yao yameandikwa katika kitabu kile cha uzima cha Mwanakondoo,wametukuzw,naam, wametukuzwa sana, yaani, kuwa washirika wa wokovu, warithi wa Mungu na warithi-wenzi pamoja na Yesu Kristo katika urithi ule usionyauka milele.

Je! huko tutakuita kuwa ni kujitoa mhanga kwa upande wetu tunapoachana na makosa na kuipokea kweli, tunapoachana na giza kwa ajili ya kuipokea nuru, tunapoachana na dhambi kwa ajili ya  kuipokea haki, tunapoachana na jina lisilodumu na urithi wa hapa duniani kwa ajili ya heshima zile za milele na milele, pamoja na hazina ile isiyo na waa lo lote ambayo hainyauki kamwe? Hata  katika maisha haya, Mkristo anaye Mmoja ambaye anaweza kumtegemea kwa msaada, ambaye atamsaidia kustahimili maonjo yake yote.

Lakini yule mwenye dhambi analazimika kustahimili maonjo yake akiwa peke yake. Anaingia kaburini kwenye giza akiwa na majuto makali, akiwa mfungwa wa Shetani, maana yeye ni mateka wake halali.... 

Kama kuna mtu ye yote ambaye angekuwa na shukrani daima, basi, mtu huyo ni yule mfuasi wa Kristo. Kama kuna mmoja anayefurahia raha ya kweli, hata katika maisha haya, basi, ni Mkristo yule aliye mwaminifu.... 

Kama sisi tukiuthamini au kuwa na fahamu  yo yote ya kujua jinsi wokovu wetu ulivyonunuliwa kwa gharama kubwa mno, basi, cho chote tunachoweza kukiita kujitolea mhanga kitazama chini kisiweze kuonekana kama kitu chenye maana yo yote ile. Letter 18, 1859.
**************************

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Toa maoni hapa...