Jumamosi, 25 Julai 2015

LESONI 5:- WAMISIONARI UHAMISHONI - Julai 25 - 31, 2015

Sabato Mchana

Somo la Juma Hili: Danieli 1-12; Isaya 39:5-7; Danieli 2:44; Mathayo 24:14,15; Mwanzo 41.
Fungu la Kukariri: “‘Naye akapewa mamlaka, na utukufu, na ufalme, ili watu wa kabila zote, na taifa zote, na lugha zote, wamtumikie; mamlaka yake ni mamlaka ya milele, ambayo hayatapita kamwe, na ufalme wake ni ufalme usioweza kuangamizwa. ’” (Danieli 7:14).

Kama watu wa unabii, Waadventista wa Sabato huamini katika kurudi upesi kwa Yesu Kristo. Kuja kwake kutaifikisha dunia hii katika mwisho wake, na kuanzisha zama mpya ya ufalme wa milele wa Mungu, kama ilivyoelezwa ifuatavyo katika kitabu cha Danieli: “Na ufalme, na mamlaka, na ukuu wa ufalme, chini ya mbingu zote, watapewa watu wa watakatifu wake Aliye juu; ufalme wake ni ufalme wa milele, na wote wenye mamlaka watamtumikia na kumtii” (Dan. 7:27). Ufalme huu ndivyo utimilifu wa imani yetu; ni kile ambacho kitabu cha Waebrania (Ebr. 11:16) inakiita “nchi iliyo bora”, ambayo watu wote wa Mungu wa vizazi vyote waliisubiria kwa hamu, ambayo “mwenye kuubuni na kuujenga ni Mungu” (Waebrania 11:10).

Lakini kitabu cha Danieli pia ni kama mwongozo wa shughuli za umisionari. Katika kitabu hicho tunaweza kupata masomo kuhusu namna Mungu alivyoweza kuwatumia baadhi ya watu kushuhudia kwa wale waliokuwa katika ujinga wa kiroho na kiteolojia. Kupitia uaminifu wao na bidii yao, na imani thabiti, waumini hawa waliudhihirisha ukweli wa Mungu aliye hai kwa wale waliojua tu miungu ya uongo, na hivyo wakawapatia wale wapangani nao fursa ya kuwa na nafasi katika ufalme wa milele.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni

Toa maoni hapa...